KWA NINI KOBE HUTEMBEA POLEPOLE?

1

Unamjua Kobe? Ushawahi kujiuliza kwa nini ana nyumba ngumu mgongoni? Halafu kwa nini anatembea polepole? Tulia! Chukua popcorn zako halafu andamana nami hadi Nchi ya Mabawa ili kupata majibu ya maswali hayo. Twen'zetu...

2

Hapo zamani za kale kobe alikuwa na gamba (wengine huita nyumba) jembamba sana. Gamba hilo lilikuwa jembamba kama makali ya wembe na jepesi kama karatasi ya gazeti.

3

Wembamba na wepesi wa gamba vilimfanya kobe awe miongoni mwa viumbe wenye kasi zaidi duniani. Alikuwa akishikilia rekodi mbalimbali za mbio ndefu na mbio fupi. Kila aliposhiriki mbio alivunja rekodi zake mwenyewe.

4

Ingekuwa ni zama hizi si shaka angalikuwa na shehena ya tuzo na medali za Olimpiki kabatini kwake. Na pengine wanyama wenzake wangelikuwa wakimwita Usain Bolt of the Jungle. Hapa nimechomekea tu.

5